VIPAUMBELE 17 KULETA MAGEUZI SEKTA YA SHERIA TANZANIA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wizara ya Katiba na Sheria imebainisha vipaumbele 17 ambavyo vitaleta mageuzi katika sekta ya sheria nchini Tanzania kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni pamoja na mageuzi ya mfumo wa kisheria katika haki jinai na haki madai na ujenzi wa miundombinu ya upatikanaji haki.
Vipaumbele hivyo vimebainishwa bungeni jijini Dodoma Ijumaa 24 Aprili 2026 na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera wakati akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Dkt. Homera amesema Wizara, Taasisi zake na Mhimili wa Mahakama itaendelea kuboresha utoaji wa huduma za kisheria na mifumo ya upatikanaji wa haki kwa umma kwa wakati na usawa ili kuendana na mipango ya sekta ya Sheria nchini na mipango ya kikanda na kimataifa ili kufikia malengo yaliyopangwa kwa kipindi husika.
Ametaja vipaumbele vingine kuwa ni kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya jinai na madai, Kuimarisha huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi na kuimarisha haki za binadamu na utawala bora nchini.
Pia kuimarisha masuala ya kikatiba na elimu ya uraia, kuimarisha uwezo kwa wataalam wa sekta ya sheria, kuimarisha huduma za ufilisi na udhamini, kuendeleza matumizi ya Kiswahili katika sekta ya sheria, Kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, kuimarisha ulinzi wa utajiri asili na maliasilia za nchi pamoja na kulinda maslahi ya Taifa.
Aidha Dkt. Homera amebainisha vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na Kuimarisha uwajibikaji na utendaji katika sekta ya sheria, mageuzi ya kidigitali katika sekta ya sheria na Ulinzi wa watoa taarifa na mashahidi.
Aliongeza kuwa vipaumbele vingine ni Mageuzi ya sheria kwa ajili ya uwekezaji na uchumi, kusimamia ajira, uteuzi, nidhamu na maadili ya watumishi wa mahakama na kuimarisha mapitio, tafiti na tathmini za sheria ili kurahisisha utekelezaji wa DIRA 2050.
Mpango na Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria 2026/27 umejengwa katika muktadha mpana wa kimkakati wa Taifa unaolenga kuiwezesha Tanzania kufikia hadhi mpya ya maendeleo, utulivu na ushindani wa kimataifa kuelekea maendeleo endelevu ya Taifa na mtu mmoja mmoja.

No comments: