VETA YATAKIWA KUSHIRIKIANA NA VIWANDA NA KUKUZA UJUZI WA VIJANA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Na Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, ameihimiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na viwanda ili kuongeza fursa za ajira na ujuzi kwa vijana nchini.
Wito huo umetolewa Aprili 23, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya ufundi wa aluminium na ufungaji wa vioo kwa wakufunzi pamoja na mafundi wa fani ya useremala.
Tukio hilo pia limeambatana na uzinduzi wa mtaala mpya wa mafunzo hayo unaoendeshwa na kampuni ya Emirates Aluminium Profile kwa kushirikiana na VETA, ukiwa na lengo la kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Wanu alisema hatua hiyo inaendana na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha rasilimali watu sambamba na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi na teknolojia duniani.
“Ushirikiano kati ya vyuo vya VETA, sekta ya uzalishaji, waajiri na viwanda ni muhimu ili kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji halisi ya soko la ajira,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema mafunzo kwa wakufunzi ni hatua muhimu katika kuboresha ubora wa ufundishaji na kuongeza ushindani wa wahitimu katika soko la ajira.
Kasore alisema awamu ya kwanza ya mafunzo hayo imehusisha wakufunzi 18 wa fani ya useremala watakaopatiwa ujuzi wa vitendo unaohitajika viwandani.
Alifafanua kuwa washiriki hao watajengewa uwezo katika maeneo mbalimbali ikiwemo makadirio ya vifaa na gharama, uundaji wa miundo ya aluminium, ufungaji wa vioo, utengenezaji wa samani za chuma pamoja na ufungaji wa dari.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Emirates Aluminium Profile, Deogratius Marandu, alisema mafunzo hayo yataongeza thamani kwa mafundi na kuwapa utambuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Marandu aliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha vijana kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Wadau wa elimu wameeleza kuwa ushirikiano kati ya VETA na sekta binafsi ni njia sahihi ya kuzalisha vijana wenye ujuzi wa kisasa unaoendana na mahitaji ya soko la ajira nchini.
No comments: