MELI KONGWE YA MV LIEMBA KUREJEA ZIWA TANGANYIKA JULY MWAKA HUU
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wananchi wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa wanatarajia kunufaika mara baada ya kukamilika kwa ukarabati wa Meli ya Kihistoria ya MV. Liemba inayotarajiwa kurejea rasmi kutoa huduma Julai 2026 katika mwambao wa Ziwa Tanganyika ambapo hadi mwanzoni mwa mwezi Mei imefikia asilimia 70
Kukamilika kwa meli hiyo kongwe na muhimu kwa uchumi wa ukanda wa Magharibi ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji, kuchochea biashara na kuinua maisha ya wananchi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika.
MV. Liemba ambayo ilisimamisha safari zake mwaka 2018 kutokana na uchakavu wa mitambo na miundombinu yake, ipo kwenye hatua za mwisho za ukarabati mkubwa ulioanza Julai 2024 kwa gharama ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 13, huku ukitarajiwa kukamilika Julai 2026.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Meneja wa Mradi, Elias Kivara, amesema ukarabati wa meli hiyo umefikia asilimia 70 na maandalizi yote ya kukamilisha asilimia zilizobaki yamekamilika.
Amesema vifaa vyote vipya vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi tayari vimewasili, jambo linaloonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati bila kuchelewa.
“ Vifaa vyote vinavyotakiwa kufungwa kwrnye meli vimeshafika, kazi iliyobaki ni kuvifunga pamoja na kumalizia kupaka rangi, hivyo tunatarajia mwezi Juni 2026 kufanya safari ya majaribio na Julai 2026 meli itaanza rasmi safari zake,” amesema Kivara.
Kurejea kwa MV. Liemba kunatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha usafiri wa wananchi pamoja na usafirishaji wa mizigo na bidhaa mbalimbali kati ya Kigoma, Katavi, Rukwa na nchi jirani zinazotumia Ziwa Tanganyika.
Wafanyabiashara wadogo na wa kati wanatajwa kuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa huduma hiyo, kwani watapata fursa ya kusafirisha bidhaa zao kwa gharama nafuu zaidi tofauti na usafiri wa barabarani ambao mara nyingi ni wa gharama kubwa.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kivara, wafanyabiashara wengi hasa wa mazao ya chakula kutoka Kigoma, Rukwa na Katavi wamekuwa wakikumbana na changamoto ya gharama kubwa za usafirishaji, hivyo kurejea kwa meli hiyo kutasaidia kuongeza biashara, kipato na ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Mbali na huduma za usafiri, meli hiyo imeboreshwa kwa kiwango cha kisasa zaidi kwa kuwekwa viti vya kisasa, vyumba vya kulala vyenye kiyoyozi, sehemu ya burudani pamoja na huduma za vinywaji yenye uwezo wa kuwa na abiria zaidi ya 53, pamoja na kuimarisha vifaa vya usalama kwa wasafiri.
Wananchi wa ukanda huo wanaamini kuwa kurejea kwa MV. Liemba kutachochea uwekezaji, kuongeza ajira kwa vijana na kufungua fursa mpya za kiuchumi katika sekta za biashara, utalii na usafirishaji.






No comments: