DC NGUBIAGAI AONGOZA VITA DHIDI YA UVUVI HARAMU UKEREWE
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde. Christopher Ngubiagai akihutubia wananchi wa Gana katika mkutano
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndg. Vicent Mbua akizungumza na wananchi wa Gana kuachana na uvuvi haramu
Na Mwandishi Wetu - Ukerewe
Mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali za taifa na kuhakikisha sekta ya uvuvi inachangia kikamilifu ukuaji wa uchumi inaendelea kuzaa matunda, ambapo Wilaya ya Ukerewe imeendelea kuchukua hatua madhubuti dhidi ya uvuvi haramu.
Katika kuonesha dhamira hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai, Juni 18, 2026 ameongoza operesheni ya kuteketeza zana haramu za uvuvi zenye thamani ya Shilingi milioni 73,615,000 katika Kisiwa cha Gana, Kijiji cha Kamasi, Kata ya Ilangala.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha rasilimali za Ziwa Victoria zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho sambamba na kuimarisha uchumi wa wananchi wanaotegemea sekta ya uvuvi.
Akizungumza katika tukio hilo, Cde. Ngubiagai amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayejihusisha na uvuvi haramu unaoharibu mazalia ya samaki na kuhatarisha ustawi wa sekta hiyo muhimu kiuchumi.
Aidha, amewahimiza wananchi kuachana na mbinu haramu za uvuvi na badala yake kutumia fursa zilizopo katika kuongeza thamani ya mazao ya samaki kupitia usindikaji, uhifadhi bora na biashara endelevu, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Vicent Mbua, amewapongeza wananchi na wajumbe wa kamati kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuutoa katika mapambano dhidi ya uvuvi haramu.
Mbua amesema ushirikiano huo unaendana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya uvuvi inakuwa endelevu na yenye tija kwa maendeleo ya wananchi na taifa.
Amesema halmashauri itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria za uvuvi ili kulinda mapato ya halmashauri na kuhakikisha wananchi wanapata samaki bora na wa kutosha.
"Kila mvuvi anapaswa kuzingatia sheria zinazomuongoza katika shughuli zake. Serikali itaendelea kudhibiti uvuvi haramu unaoharibu mazalia ya samaki na kuhatarisha uchumi wa wananchi," amesema Mbua.
Katika taarifa yake, Katibu wa Mwalo wa Gana, Charles Gunda, amesema zana zilizoteketezwa ni pamoja na timba pisi 1,627 na nyavu za makira inchi tatu pisi 80.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ilangala, Petro Majura, ameonya kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uvuvi haramu.
Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Godfrey Ayako, amesema Serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya uvuvi ikiwemo suala la upimaji wa mizigo ya dagaa ili kuongeza ufanisi na tija kwa wavuvi.
Sambamba na juhudi hizo, Cde. Ngubiagai amewahimiza wananchi kuunda na kusajili vikundi ili waweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kiuchumi.













No comments: