HAZINA SACCOS YALENGA KUMUINUA MTUMISHI KIUCHUMI KABLA NA BAADA YA KUSTAAFU
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mtendaji Mkuu wa Hazina SACCOS, Dkt. Festo Mwaipaja amesema taasisi hiyo imejipambanua katika kuwahudumia watumishi wa Serikali na sekta binafsi kwa lengo la kuwasaidia kujiimarisha kiuchumi kabla na baada ya kustaafu.
Dkt. Mwaipaja ameyasema hayo wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Hazina SACCOS uliofanyika katika Ukumbi wa Rock City, jijini Mwanza.
Amesema wamebaini changamoto inayowakabili baadhi ya watumishi baada ya kustaafu, ambapo hukumbwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na kukosa kipato cha uhakika, hali inayowalazimu wengine kukopa mikopo yenye masharti magumu.
Amesema Hazina SACCOS imekuja kama sehemu ya suluhisho kwa kuwawezesha watumishi kupata mikopo yenye masharti rafiki, huku ikiwasisitiza kujenga utamaduni wa kuweka akiba ili kuwa na uwezo wa kujiendesha kiuchumi hata baada ya kustaafu.
“Tumekuja kama suluhisho la kuwapa watumishi mikopo rafiki ambayo wanaweza kuirejesha bila riba ndani ya mwaka mmoja” amesema Dkt. Mwaipaja.
Aidha, amewataka watumishi kujiunga na Hazina SACCOS na kuanza kuweka akiba mapema, akisisitiza kuwa utaratibu huo unaweza kumsaidia mwanachama kujenga msingi imara wa kiuchumi na kuwa na kipato cha kujitegemea baada ya kustaafu.
Dkt. Mwaipaja amesema Hazina SACCOS inatoa huduma kwa Watanzania waliopo Tanzania Bara, ikiwa na lengo la kuwafikia watumishi wengi zaidi na kuwasaidia kujenga maisha bora ya kiuchumi kupitia akiba na mikopo.
Tazama VIDEO hapa chini

No comments: