LIVE STREAM ADS

Header Ads

SERIKALI KUPITIA UCSAF YAENDELEA KUIMARISHA MTANDAO WA MAWASILIANO HASA VIJIJINI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote () imedhamiria kuwaunganisha wananchi pembezoni hasa vijijini na huduma bora za mawasiliano ikiwemo simu, intaneti, utangazaji na posta bila kujali jiografia, hali ya uchumi au kijamii.

Ili kutimiza lengo hilo tayari imeanza utekekalezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya mawasiliano ya simu ambapo hadi kufikia Aprili 2026 makubaliano yaliyopo ni kufikia Kata 2,293 zenye Vijiji 5,505 na wakazi zaidi ya milioni 32.7 pamoja na kufanikisha ujenzi wa minara 2,324 ya mawasiliano.

Akizungumza Jumatatu Agosti 10, 2026 katika mafunzo ya wahariri wa vyombo vya habari mkoani Mwanza yaliotolewa na mfuko huo,Mkuu wa Kanda ya Ziwa UCSAF- Fredy Kandonga alisema huduma imekamilika katika Kata 2,012 zenye vijiji 5,132 ambapo wakazi takribani milioni 29.7 tayari wanapata huduma kupitia minara 2,158.

Kandonga alisema kwa Kanda ya Ziwa, takribani minara 414 imejengwa katika Kata zipatazo 380 za mikoa ya Mwanza, Simiyu, Mara, Shinyanga, Geita na Kagera.

Alisema awamu ya 10 ya mradi wa mawasiliano, utekelezaji wake unaendelea katika Kata 287 zenye vijiji 359, huku minara 287 ikiendelea kujengwa ambapo wakazi takribani milioni 2.9 wanatarajiwa kunufaika.

"Ruzuku ya Serikali ni takribani shilingi bilioni 29, mradi unatarajiwa kukamilika Machi 2027. Hadi sasa minara saba imewashwa na wananchi wanapata huduma kupitia minara hiyo. Kanda ya Ziwa minara 67 inajengwa ambapo mnara mmoja tayari umewashwa"alisema Kandonga.

Pia alisema katika awamu hiyo ya 10 ya mradi wa mawasiliano kwa Kanda ya Ziwa, mkoa wa Geita inajengwa minara saba, Kagera minara 14, Mara minara 11, Mwanza minara 21, Shinyanga minara sita na Simiyu minara nane.

Alisema mradi huo unawezesha matumizi ya elimu mtandao, afya mtandao, biashara mtandao na huduma za kifedha kupitia simu ambapo minara 431 imeboreshwa kutoka 2G kwenda 2G/3G/4G huku ruzuku ya Serikali ikiwa ni shilingi bilioni 9.14.

"UCSAF itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya umma na binafsi kufikia Tanzania ya kidijitali. Tupo tayari kushirikiana na wadau wote wakiwemo Wahariri wa Habari ili kubaini na kutatua changamoto za mawasiliano nchini" alisisitiza Kandonga.

No comments:

Powered by Blogger.