LIVE STREAM ADS

Header Ads

REDESO, VETA WAFUNDISHA WAKUFUNZI NISHATI SAFI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Shirika la Relief to Development Society (REDESO) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) limetoa mafunzo kwa wakufunzi 12 kutoka vyuo vya VETA kuwa wakufunzi wa wakufunzi (Trainers of Trainers - ToT) katika teknolojia za nishati safi.


Wakufunzi hao wanatoka katika vyuo vya VETA vya Dar es Salaam, Moshi, Mbeya, Mwanza, Pwani na Singida, na wanashiriki mafunzo ya siku 10 yanayochanganya nadharia na vitendo kwa lengo la kuwaongezea ujuzi kuhusu teknolojia za nishati safi.

Mradi huo unalenga kuwawezesha wanawake na vijana kupata ujuzi wa vitendo kuhusu nishati safi, ukijikita katika teknolojia kuu tatu ambazo ni nishati ya jua, majiko banifu ya nishati safi na usafiri unaotumia umeme, ikiwamo magari, pikipiki na bajaji za umeme.

Mafunzo hayo yanahusisha mifumo ya nishati ya jua, vifaa vyake pamoja na namna ya kufunga mifumo hiyo majumbani. Mafunzo ya vitendo yanaendeshwa na mtaalamu wa teknolojia ya nishati ya jua, Mzumbe Musa, anayewaongoza washiriki kuhusu ufungaji, matumizi na matengenezo sahihi ya mifumo ya umeme wa jua.

Mafunzo hayo yanafanyika katika Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro. Baada ya kukamilisha mafunzo hayo, wakufunzi hao 12 watapeleka maarifa na ujuzi walioupata kwa wanafunzi wao.

REDESO na VETA pia zimeandaa mtaala wa nishati safi ambao utaingizwa katika mitaala ya vyuo vya TVET vinavyoshiriki, ili kuhakikisha ujuzi kuhusu nishati safi unakuwa sehemu ya mafunzo ya kawaida ya ufundi stadi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkufunzi wa VETA Moshi, Mhandisi Frank Kabipi, amesema mafunzo hayo yameongeza uelewa wake kuhusu teknolojia za nishati safi na yatamwezesha kuwafundisha wanafunzi ambao baadaye watapeleka maarifa hayo kwa jamii.

“Mafunzo haya ni muhimu kwa maendeleo yangu binafsi na kwa jamii yangu kwa sababu dunia inahama kutoka kwenye nishati zinazochafua mazingira kwenda kwenye nishati safi kwa ajili ya kulinda mazingira. Sasa tutawafundisha wanafunzi namna ya kufunga mifumo ya umeme wa jua, majiko banifu na vifaa vya usafiri vinavyotumia nishati safi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa VETA Dodoma, Bahati Kaniki, alisema mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa matumizi mbalimbali ya nishati ya jua, ikiwa ni pamoja na kupikia, usafiri na kupata mwanga.

“Nimejifunza kwa vitendo na sasa nitakwenda kuwafundisha wanafunzi wangu ili waweze kutumia teknolojia hizi na kupeleka maarifa hayo katika jamii,” alisema.

Mkufunzi kutoka VETA Pwani,Ezekiel Shili amesema mafunzo hayo yatasaidia jamii kuondokana na matumizi ya nishati chafu ambayo yana madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

“Kupitia sisi walimu, ninaamini tutaleta mabadiliko chanya katika jamii zetu kwa kuwa tutawafundisha vijana na wanawake kupata maarifa kuhusu nishati safi na kuchukua hatua ya kutumia teknolojia za kupikia kwa nishati safi, vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati safi na umeme wa jua,” amesema.

Wakati huo huo, Mkufunzi wa VETA Dar es Salaam, Philemon Julius, na Mkufunzi wa VETA Mwanza, Musa Doma, wamesema mafunzo hayo ni mabadiliko makubwa katika matumizi ya nishati safi.

Wamesema watatumia njia za nadharia na vitendo kuwafundisha wanafunzi wao ili kuchochea mabadiliko chanya katika jamii.

Mradi huo unaofadhiliwa na International Development Research Centre (IDRC) unalenga kuongeza uelewa na ujuzi wa vitendo kuhusu matumizi ya nishati safi, kupunguza hewa ukaa na kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Mzumbe, mfumo wa mafunzo kwa wakufunzi unalenga kuleta matokeo mapana kwa kuwawezesha wakufunzi kupata ujuzi ambao watawafikishia wanafunzi, wanawake na vijana wengi zaidi, na hivyo kuongeza matumizi ya teknolojia za nishati safi katika jamii.

No comments:

Powered by Blogger.