LIVE STREAM ADS

Header Ads

SHIRIKA LA HAKIRASILIMALI LATOA MAFUNZO KWA WANAHABARI, WADAU WA UCHIMBAJI MDOGO WA MADINI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la HakiRasilimali limetoa mafunzo kwa wanahabari na wadau wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji wadogo wa dhahabu na viongozi wa asasi za kirahia ili kuwajengea uwezo wa kutumia taarifa na ushahidi katika kuchambua masuala yanayohusu uchimbaji mdogo wa madini (ASM).

Mafunzo hayo ya siku mbili kuanzia Jumatatu Septemba 29, 2026 yamefanyika mkoani Geita, yakilenga kuongeza uelewa kwa washiriki kuhusu masuala ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji (madini, mafuta na gesi).

Akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo, Mkuu wa Sehemu ya Utafiti wa kutoka taasisi ya Tanzania Extractive Industries Transparency Initiative (TEITI), Andrew Eriyo amesema ripoti za kila mwaka za taasisi hiyo zikitumika ipasavyo zinaweza kusaidia kuleta mabadiliko katika sekta ya madini ikiwemo sheria, sera, uwazi na uwajibikaji kwa jamii.

Amesema taasisi hiyo imekuwa ikisaidia upatikanaji wa taarifa, kuhimiza kampuni kutoa taarifa sahihi na kufanya ulinganishi wa taarifa za mapato na malipo kati ya kampuni na Serikali hatua inayosaidia kubaini tofauti zinazoweza kujitokeza katika taarifa zinazowasilishwa na pande hizo.

Eriyo amesisitiza umuhimu wa wanahabari kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) inayotekelezwa na kampuni za madini na kampuni nyingine za uziduaji ili kusaidia jamii kunufaika na miradi hiyo.

Amesema ufuatiliaji huo unapaswa kuangalia kama miradi inayotekelezwa kama inaendana na makubaliano yaliyowekwa kulingana na mahitaji na vipaumbele vya jamii zinazozunguka maeneo ya shughuli za uchimbaji madini.
Mkuu wa Sehemu ya Utafiti TEITI, Andrew Eriyo, akizungumza na washiriki kuhusu uwazi, uwajibikaji na matumizi ya taarifa katika sekta ya madini.

Naye Meneja Miradi wa HakiRasilimali, Lucy Shao amewataka waandishi wa habari kuzingatia ushahidi katika kuandaa habari zenye maslahi kwa jamii.

Shao amesema taarifa kutoka kwa chanzo kimoja pekee haiwezi kuchukuliwa moja kwa moja kuwa ushahidi, hivyo wanahabari wanapaswa kuwa na uwezo wa kutafuta taarifa, kuzihakiki na kuzihusianisha na ushahidi mwingine kabla ya kufikia hitimisho la kuchapishwa.

Ameongeza kuwa taarifa zinazotolewa na TEITI, ikiwemo ripoti zinazohusu sekta ya wachimbaji wadogo, zinaweza kutumika kama nyenzo muhimu katika utafiti wa habari na kuwasaidia waandishi kuibua maswali yanayohitaji uchunguzi zaidi.
Meneja Miradi wa HakiRasilimali, Lucy Shao, akieleza umuhimu wa ushahidi na uhakiki wa taarifa katika uandishi wa habari.

Kwa upande wake Wakili wa Kujitegemea kutoka Himiza Social Justice, Gerald Makungulu amesema mtazamo wa kisheria kuhusu upatikanaji na matumizi ya taarifa katika masuala yanayohusu sekta ya madini na maslahi ya umma unapaswa kuthibitishwa bila kuacha shaka kabla ya kutumika na asasi ama wanahabari ili kuepuka mvutano wa kisheria.
Afisa Mradi kutoka taasisi ya HakiRasilimali, Irene Mosha.

Akiwasilisha mada kuhusu habari za uchunguzi, Mhariri Mwandamizi, Ephrahim Bahemu amewakumbusha wanahabari kuhusu umuhimu wa kuzingatia misingi ya taaluma katika uandishi wa habari za uchunguzi ili kuepuka matishio ya kiusalama.

Bahemu amesema mwandishi anapaswa kuhakikisha anapata ushahidi wa kutosha, kuhakiki taarifa na kutoa nafasi kwa pande zote zinazohusika kabla ya kuchapisha habari, hususani habari zinazogusa masuala yenye maslahi mapana kwa umma.

Amesema uandishi wa habari za uchunguzi una nafasi muhimu katika kufuatilia matumizi na usimamizi wa mali za umma, akiwataka waandishi kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi na kutumia takwimu katika kazi zao hasa za uchunguzi.
Mhariri Mwandamizi, Ephrahim Bahemu akizungumza kuhusu misingi ya uandishi wa habari za uchunguzi kwa njia ya mrandao.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa katika majadiliano.
Mafunzo hayo yamejumuisha washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Geita.

No comments:

Powered by Blogger.