LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kambi ya madaktari bingwa kutoa huduma bure jijini Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wakazi wa Jiji la Mwanza wanatarajiwa kupata huduma za matibabu bure katika kambi maalum ya madaktari bingwa na bobezi itakayofanyika kuanzia Oktoba 09 hadi 12, 2026 katika uwanja vya Nyamagana.

Kambi hiyo imeandaliwa na Mbunge wa Nyamagana, John Nzilanyingi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza.

Akizungumza Septemba 29, 2026 na waandishi wa habari, Nzilanyingi amesema kambi hiyo inalenga kuwapatia wananchi huduma za uchunguzi, matibabu na elimu ya afya.

Amesema pia kambi hiyo ni sehemu ya kutoa shukrani kwa wakazi wa Mwanza kwa kumchagua kuwa Mbunge wa Nyamagana.

Madaktari watakaoshiriki wanatoka India pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Hospitali ya Kanda ya Bugando, Sekou-Toure na Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana.

Huduma zitakazotolewa ni pamoja na uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo, saratani, kisukari, shinikizo la damu, mifupa na maumivu ya mgongo.

Huduma nyingine ni za magonjwa ya figo na mfumo wa mkojo, tezi dume, mfumo wa fahamu, ini, ngozi, mfumo wa upumuaji na utumbo.

Pia kutakuwa na huduma za afya ya wanawake na uzazi, watoto, upasuaji, vipimo, ushauri wa kibingwa na rufaa kwa wagonjwa watakaohitaji matibabu zaidi.

Wananchi wametakiwa kuanza kujiandikisha katika zahanati zilizo karibu nao, vituo vya afya vya Mkolani, Bulale, Igoma na Fumagila na Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana.

Nzilanyingi amesema huduma zote katika kambi hiyo zitatolewa bure na hakutakuwa na muda wa nyongeza baada ya kambi kumalizika Oktoba 12, 2026.
Wanahabari.
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, John Nzilanyingi.

No comments:

Powered by Blogger.