WATANZANIA WAASWA KUJITOKEZA KUSHIRIKI MCHEZO WA 'PICKLEBALL'
WATANZANIA wametakiwa kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika mchezo wa Pickleball kwa lengo la kuibua na kukuza vipaji vipya vitakavyoiwezesha Tanzania kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Dkt. Sajad ambaye pia ni Meneja Mkazi wa Mansoor Industries LTD, amesema mchezo wa Pickleball ambayo kadri siku zinavyokwenda unazidi kujichukulia umaarufu ndani na nje ya Tanzania, unapaswa kuchukuliwa kwa umuhimu Mkubwa na watanzania wote.
" Ni vyema watanzania sasa tukaona umuhimu wa mchezo huu, tunatakiwa kuuona kama michezo mingine ambayo imeweza kuliletea heshima kubwa Taifa letu, pamoja na hayo mchezo huu kama michezo mbalimbali inasaidia kulinda na kujenga afya ya mwili", amesema Dkt. Sajad.
Aidha ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo chini ya Waziri wake Paul Makonda 'kuubeba', kuunyanyua na kuukuza mchezo huo wa Pickleball ili uweze kukuletea tija kwa Taifa hili.
Kwa upande wake Mratibu na Kocha wa Mchezo huo hapa nchini Abdallah Manyua amesema mchezo huo una faida mbalimbali kiafya na kijamii, huku akitoa rai kwa Serikali na Watanzania kuendelea kuunga mkono na kushiriki mchezo huo unaozidi kupata umaarufu.
Amesema tangu kuingia kwa mchezo nchini wadau mbalimbali wamejitokeza na kuonesha mapenzi nao huku akitumia nafasi hiyo kuishukuru Dkt. Sajad Habib Rai kwa ushirikiano anaoutoa ambao unasaidia kukua kwa mchezo huo.
Mmiliki wa uwanja wa Pickleball Smashzone na mdau wa michezo nchini, Idris Dosaji, amesema wameamua kuwekeza katika uwanja huo kutokana na umuhimu wa kutoa nafasi kwa wananchi kujifunza na kushiriki mchezo huo.
Aidha, amewahimiza wananchi kujitokeza na kutumia fursa hiyo kushiriki Pickleball kwa ajili ya afya na burudani.






No comments: