WANAWAKE KUTOKA JAMII ZA ASILI WAJENGEWA UWEZO KUTETEA HAKI ZA ARDHI
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wanawake kutoka jamii za asili nchini wamepewa mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuimarisha utetezi wa haki za ardhi.
Mafunzo hayo pia yametoa fursa kwa wanawake kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu za kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika umiliki na usimamizi wa ardhi za jamii.
Zaidi ya wanawake 35 kutoka mikoa mbalimbali nchini wameshiriki mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro, yakilenga kuwawezesha wanawake kutambua changamoto za ardhi zinazowakabili na kuimarisha nafasi yao katika kutetea haki zao za umiliki na usimamizi wa rasilimali za pamoja.
Mafunzo hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano wa mashirika ya Green Conservers, WoMin na Kinnapa na kutoa fursa kwa wanawake wanaojihusisha na urejeshaji na usimamizi wa ardhi za jamii pamoja na usimamizi na ugawaji wa rasilimali za mifumo ikolojia, kukabiliana na vikwazo vinavyowazuia kupata na kusimamia haki zao za ardhi.
Akizungumzia umuhimu hayo, Nengai Godfrey kutoka shirika la Green Conservers alisema yatawasaidia wanawake kujifunza kutoka kwa wenzao kuhusu mbinu zinazoweza kutumika kutatua changamoto za umiliki wa ardhi na kuimarisha nafasi ya wanawake katika kutetea haki zao.
"Matarajio yetu ni kwamba wanawake hawa watatumia ujuzi waliopata kutoka kwa wanawake wenzao, waliobadilishana nao uzoefu kutoka maeneo mbalimbali katika kusimamia nafasi ya mwanamke kwenye kupambania haki katika jamii" alisema Nengai.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema maarifa na uzoefu walioupata vitawasaidia kuimarisha utetezi wa haki za wanawake katika umiliki na usimamizi wa ardhi, na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili katika jamii zao.
Miongoni mwa washiriki hao ni Hellen Keia kutoka Simanjiro ambaye alisema mafunzo hayo yamemuongezea maarifa na mbinu zitakazomsaidia kuimarisha utetezi wa haki za wanawake katika masuala ya umiliki wa ardhi.
Kwa upande wake, Innocensia Lawrence kutoka Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, alisema mafunzo hayo yatasaidia kutatua migogoro wa ardhi kati ya wanajamii hasa wanawake na mwekezaji kwani wamewawezesha kuwa na uelewa na mbinu za kukabiliana na changamoto za ardhi.
Lawrence aliongeza kuwa kupitia mafunzo hayo ya siku tatu, washiriki wamepata mbinu zaidi za kutetea haki za wanawake na kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika umiliki na usimamizi wa ardhi.
Mbali na mafunzo ya darasani na kubadilishana uzoefu, washiriki pia walitembelea jamii mbili mkoani Morogoro kwa lengo la kujifunza kuhusu nafasi ya wanawake katika jamii hizo, changamoto wanazokabiliana nazo katika masuala ya ardhi na mbinu zinazoweza kutumika kukabiliana na changamoto hizo.
Ziara hiyo ya kimafunzo iliwasaidia washiriki kujifunza kutokana na uzoefu wa jamii nyingine na kutafakari namna maarifa waliyoyapata yanavyoweza kutumika kuimarisha utetezi wa haki za ardhi katika maeneo yao.












No comments: