Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog, Dodoma
Jamii imetakiwa kutofumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao, kwa kutoa taarifa na kuchukua hatua zinazostahili ili kulinda wanawake na watoto na kujenga familia, jamii na taifa imara.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Athuman Katimba, wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, uliofanyika Novemba 25, 2026, jijini Dodoma.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Tuungane Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto: Jenga Taifa Imara Lenye Haki na Usawa Kuelekea Dira 2050.”
Katimba amesema Serikali inaendelea kutekeleza programu na kampeni mbalimbali zinazolenga kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ikiwemo Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) na Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili (2024/25–2028/29).
Amesema Serikali pia imetekeleza afua mbalimbali za kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya ukatili, ikiwemo Kampeni ya Kitaifa ya Kulinda Watoto dhidi ya Matumizi ya Mtandao, uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika Jeshi la Polisi, vyuo vikuu na vyuo vya kati, pamoja na madawati katika maeneo ya umma kwa ajili ya kutoa huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.
“Mipango, programu na kampeni hizi zinalenga kusaidia utekelezaji wa Dira 2050 ili kuhakikisha mtaji watu wa kuleta maendeleo unalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili,” amesema Katimba.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi amesema mapambano dhidi ya ukatili yanahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali ili kuongeza nguvu na kuondoa vitendo hivyo katika jamii.
Amesema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kuendana na utekelezaji wa Dira 2050 kupitia Jamii Ajenda 2050, inayolenga kujenga familia imara, jamii imara na taifa imara.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu, amesema Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia inaunganisha wadau mbalimbali katika kupambana na changamoto hiyo.
Amesema mkoa umeifanya ajenda ya kupinga ukatili kuwa sehemu ya vipaumbele vyake kwa kushirikiana na wataalamu na wadau mbalimbali kutoa elimu, kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa za ukatili na kuhimiza ushirikiano wa taasisi zinazohusika na mapambano hayo.
ANNA KULAYA ATAJA MAENEO SITA YA KIPAUMBELE
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (Mkuki) unaojumuisha mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 200 chini ya uratibu wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) , Mratibu wa Kitaifa wa WiLDAF Tanzania, Wakili Anna Kulaya, ameiomba Serikali kuyafanyia kazi maeneo sita ya kipaumbele yanayolenga kuimarisha ulinzi wa wanawake na watoto, kuzuia ukatili na kuhakikisha manusura wanapata haki.
Mratibu wa Kitaifa wa WiLDAF Tanzania, Wakili Anna Kulaya.
Kulaya amesema mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hayapaswi kupimwa kwa ukuaji wa uchumi, miundombinu na teknolojia pekee, bali pia namna wananchi wanavyoishi katika usalama, wanavyolindwa na kufurahia haki zao.
Amesisitiza kuwa usawa wa kijinsia, haki na utu wa binadamu ni misingi muhimu ya maendeleo, akieleza kuwa taifa haliwezi kuwa imara wakati wanawake wanaishi kwa hofu ya ukatili, watoto hawako salama na wanawake wajane wanapoteza haki zao za kumiliki na kurithi mali.
Akifafanua maeneo hayo, amesema la kwanza ni kulinda uhai wa wanawake na kutokomeza mauaji yanayohusiana na jinsia (Femicide). Amesema baadhi ya wanawake wamekuwa wakikabiliwa na vitisho na ukatili ndani ya mahusiano yao, hali inayoweza kuongezeka na kusababisha vifo.
Amesema Serikali inapaswa kuweka mkakati mahsusi wa kuzuia mauaji hayo, kuanzisha mfumo wa ukusanyaji wa takwimu, kuimarisha utambuzi wa viashiria vya hatari, kutoa ulinzi wa haraka na kuhakikisha uchunguzi pamoja na uwajibikaji kwa mujibu wa sheria.
Amesisitiza kuwa mifumo ya ulinzi inapaswa kuchukua hatua mwanamke akiwa hai badala ya kusubiri maisha yake yapotee.
Eneo la pili ni kutungwa kwa Sheria Mahsusi na Jumuishi ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia. Kulaya amesema ukatili wa kijinsia hauishii katika kupigwa au kubakwa pekee, bali unahusisha pia udhibiti wa kiuchumi, vitisho, udhalilishaji wa kisaikolojia, ukatili wa kingono na ukatili unaowezeshwa na teknolojia.
Ameiomba Wizara ya Katiba na Sheria, kwa kushirikiana na wizara na taasisi husika, kuharakisha mchakato wa kutunga sheria hiyo kwa kuzingatia pia Sheria ya Mfano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu Ukatili wa Kijinsia.
Amesema sheria hiyo inapaswa kuweka mfumo madhubuti wa kuzuia ukatili, kutoa amri za ulinzi, kuhakikisha huduma jumuishi kwa manusura na kuweka wajibu wa wazi kwa taasisi zinazohusika.
Eneo la tatu ni kutokomeza adhabu ya viboko na kulinda utu wa watoto. Kulaya amesema watoto wanapopelekwa shuleni wanatarajiwa kupata elimu katika mazingira salama, hivyo adhabu zinazoweza kuwasababishia majeraha, hofu na maumivu zinapaswa kuangaliwa upya.
Amesema wanachama wa MKUKI wameupokea kwa matumaini uamuzi wa Mahakama Kuu wa Novemba 3, 2026, katika shauri la Samweli Maduhu Mangu dhidi ya Waziri wa Elimu na mwingine, kuhusu adhabu ya viboko shuleni.
Hata hivyo, amesema wamepokea kwa masikitiko taarifa ya nia ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, huku akiitaka Serikali kutafakari upya hatua hiyo kwa kuzingatia maslahi bora ya mtoto.
Aidha, ameitaka Serikali kufanya mapitio ya sheria, kanuni na miongozo inayoruhusu adhabu ya viboko, kuweka mkakati wa kuzitokomeza katika mazingira yote na kuwajengea uwezo walimu, wazazi na walezi kutumia mbinu za nidhamu chanya.
Eneo la nne ni kukamilisha marekebisho ya Sheria ya Ndoa, Sura ya 29. Kulaya amesema Serikali inapaswa kuweka umri wa chini wa ndoa kuwa miaka 18 kwa wasichana na wavulana, bila mianya inayoruhusu ndoa za utotoni.
Ameeleza kuwa mwaka 2019, Mahakama ya Rufani katika shauri la Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebeca Z. Gyumi ilithibitisha uamuzi kuhusu kutokubalika kikatiba kwa masharti yanayoruhusu wasichana walio chini ya miaka 18 kuolewa.
Amesema mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu, kujenga ndoto zake na kuamua mustakabali wa maisha yake, hivyo haki hiyo haipaswi kuzuiwa na umaskini, mila au matarajio ya kijamii.
Eneo la tano ni mageuzi ya sheria za mirathi na urithi. Kulaya amesema Serikali inapaswa kuharakisha mapitio na marekebisho ya sheria hizo, ikiwemo masharti ya sheria za kimila zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 436 la mwaka 1963, ili kuondoa ubaguzi wa kijinsia.
Amesema kuna wanawake ambao baada ya kufiwa na wenza wao hukumbana na changamoto za kunyang'anywa mali na kupoteza haki ya kuendelea kuishi katika nyumba walizoshiriki kujenga.
Amesisitiza kuwa mwanamke hapaswi kupoteza usalama wake wa kiuchumi kwa sababu amefiwa na mwenza wake, bali haki yake ya kumiliki na kurithi mali inapaswa kulindwa na sheria.
Eneo la sita ni kuimarisha upatikanaji wa haki na huduma kwa manusura wa ukatili. Kulaya amesema ni muhimu kuhakikisha kuwa wanawake na watoto wanapotoa taarifa za ukatili wanapata ulinzi na huduma zinazohitajika bila vikwazo.
Amezitaka mamlaka kuimarisha Madawati ya Jinsia na Watoto ya Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha yana watumishi wenye ujuzi, vifaa, bajeti na mazingira yanayolinda usiri na utu wa manusura.
Pia ameitaka Serikali kuongeza vituo vya huduma jumuishi (One Stop Centres) na nyumba salama katika maeneo mbalimbali nchini, pamoja na kuhakikisha huduma za afya, msaada wa kisheria na kisaikolojia zinapatikana bila vikwazo vya kiuchumi, kijiografia au ulemavu.
Amesisitiza umuhimu wa mashauri ya ukatili kushughulikiwa kwa wakati, manusura na mashahidi kulindwa dhidi ya vitisho na kutengwa kwa bajeti mahsusi na za kutosha kwa ajili ya kuzuia na kushughulikia ukatili wa kijinsia katika ngazi zote.
Katika hatua nyingine, Kulaya amependekeza Wizara ya Katiba na Sheria, kwa kushirikiana na wizara na taasisi nyingine husika, kuweka utaratibu wa pamoja na Mtandao wa MKUKI wa kufanyia kazi maeneo hayo sita.
Amesema utaratibu huo unapaswa kuwa na hatua mahsusi, muda wa utekelezaji, rasilimali na taasisi zitakazowajibika ili kuhakikisha mapendekezo hayo yanazaa matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.
Amesema wanaharakati wako tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa ushahidi, kuchangia utaalamu na kushiriki katika michakato ya mageuzi, huku wakiendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi na maamuzi yanayofanywa.
Kulaya amesema Tanzania inayotarajiwa kufikiwa mwaka 2050 inapaswa kuwa taifa ambalo mwanamke anaishi bila hofu ya ukatili, mtoto anakua katika mazingira salama, msichana anatimiza ndoto zake, mjane analindwa dhidi ya uporaji wa mali na kila manusura anapata haki na huduma bila ubaguzi.
“Haki za wanawake na watoto ni za leo. Wanawake hawahitaji huruma badala ya haki, watoto hawahitaji ukatili ili kujengewa nidhamu, na taifa halihitaji ahadi zisizoambatana na utekelezaji,” amesema Kulaya.
No comments: