LIVE STREAM ADS

Header Ads

CRDB YAUNGA MKONO JITIHADA ZA SERIKALI KUBORESHA ELIMU MISUNGWI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, Benki ya CRDB Kanda ya Ziwa imekabidhi madawati 40 katika Shule ya Sekondari Chief Ilago iliyopo Kata ya Usagara, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo Ijumaa Oktoba 30, 2026, Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Denis Mwoleka, alisema benki hiyo imekuwa na mwendelezo wa kutoa madawati katika shule mbalimbali za msingi na sekondari ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.

Mwoleka alisema baada ya kuona Serikali ikiwekeza katika ujenzi wa madarasa, CRDB ilianzisha kampeni ya 'Keti Jifunze' kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa madawati na hivyo kuboresha mazingira ya wanafunzi kujifunzia.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Misungwi, Abdi Makange, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Johari Samizi, aliipongeza CRDB kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha wanafunzi chini wanapata elimu bora.

"Elimu bora ni pamoja na kuwa na miundombinu mizuri kama madawati na madarasa, lakini CRDB mmekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mnasaidia Serikali katika utekelezaji wa miundombinu hiyo" alisema Makange.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Chief Ilago, Abdallah Juma, alisema shule hiyo ina upungufu wa madawati 360, hivyo madawati 40 yaliyotolewa yatasaidia kupunguza changamoto hiyo.

Kwa upande wake, Winfrida Zacharia Magida, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, aliishukuru CRDB kwa msaada huo huku akieleza kuwa madawati hayo yataboresha mazingira yao ya kujifunzia, hatua itakayosaidia kuchochea ufaulu wao.
Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Denis Mwoleka.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Misungwi, Abdi Makange.
Wanafunzi Shule ya Sekondari Chifu Ilago wilayani Misungwi.

No comments:

Powered by Blogger.