LIVE STREAM ADS

Header Ads

ELIMU YA URAIA YATOLEWA KWA VIONGOZI, WATENDAJI SIMANJIRO

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora yaliyotolewa kwa viongozi na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, yameongeza uelewa na kuimarisha uwezo wao katika kuzingatia misingi ya utawala bora, uwajibikaji na utoaji wa huduma zenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya wananchi.

Mafunzo hayo yaliyofanyika leo, Oktoba 30, 2026, katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, washiriki wameeleza kuwa maarifa na ujuzi walioupata utakuwa chachu ya kuboresha utendaji wao, kuongeza uwajibikaji na kuleta mabadiliko chanya katika namna ya kuwahudumia wananchi.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Ruvu Remiti, Andrew Davidi, ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa amepata uelewa muhimu hususan katika eneo la ulinzi na usalama, ambao utamwezesha kuwafikishia wananchi elimu hiyo kwa lengo la kujenga jamii yenye amani, mshikamano na usalama.

Amesema mafunzo hayo yamempa maarifa yatakayomsaidia kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, huku akieleza kuwa ni muhimu viongozi na watendaji kuwaelimisha wananchi kuhusu wajibu wao katika kulinda amani na usalama wa maeneo yao, pamoja na kushirikiana na vyombo husika katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika jamii.

Kwa upande wake, Mrakibu wa Polisi wa Wilaya ya Simanjiro, Meena Elia, amepongeza mafunzo hayo akieleza kuwa yamekuja kwa wakati muafaka kwa kuwa yameongeza uelewa kuhusu wajibu wa viongozi na watendaji katika kuwahudumia wananchi.

Amefafanua kuwa huduma zinazotolewa katika vituo vya polisi zinapaswa kuzingatia mafunzo na taratibu za kiutendaji, ikiwemo misingi ya huduma kwa wateja, ili kuhakikisha wananchi wanapokelewa, wanasikilizwa na kuhudumiwa kwa heshima na weledi.

Washiriki hao wameeleza kuwa maarifa waliyoyapata yatawasaidia kuboresha namna wanavyotekeleza majukumu yao, kuimarisha uwajibikaji, kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi kwa wakati, hatua inayotarajiwa kuchochea mabadiliko katika utoaji wa huduma na kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na wananchi.

No comments:

Powered by Blogger.