LIVE STREAM ADS

Header Ads

SEKTA YA UZIDUAJI IZINGATIE UTAWALA BORA, HAKI ZA BINADAMU- MPELUMBE

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Dunford Mpelumbe, amesema uwekezaji katika sekta ya uziduaji unapaswa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinachangia ustawi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Mpembule ameyasema hayo Novemba 12, 2016 jijini Dodoma wakati akifungua Jukwaa la 11 la Uziduaji ambalo huandaliwa na shirika la HakiRasilimali.

Mpelumbe amesema katika kusimamia na kuhakikisha misingi ya utawala bora na haki za binadamu inazingatiwa na Serikali pamoja na sekta binafsi, Tume hiyo imepewa mamlaka kikatiba.

Amesema katika kutekeleza hilo, Tume hiyo imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kushirikiana na wadau kuhakikisha misingi elekezi ya Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na haki za binadamu (UNGPs) inaingizwa katika mifumo ya kitaasisi, kisheria na kisera nchini.

Amesema hatua hiyo inafanyika kupitia ushiriki wa Tume katika mchakato wa kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Biashara na Haki za Binadamu (NAP-BHR), unaotoa mwongozo wa utekelezaji wa misingi hiyo.

Mpelumbe amesema Tanzania inapitia kipindi kipya cha uwekezaji katika sekta ya uziduaji ambacho kimeongeza shughuli za uchimbaji wa madini ya kimkakati kama Nickel na Graphite, pamoja na uwekezaji katika mafuta na gesi asilia hivyo wananchi wanapaswa kuwa wanufaika.

Amesema pamoja na fursa za kukuza uchumi na kuongeza ajira zinazotokana na uwekezaji huo, ni muhimu kuhakikisha unazingatia uwazi, uwajibikaji, ulinzi wa mazingira na maslahi mapana ya taifa.

Ametaja changamoto za migogoro ya ardhi, ucheleweshaji wa fidia na athari za kimazingira kwa jamii kuwa miongoni mwa masuala yanayohitaji kushughulikiwa ili kulinda haki za wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la HakiRasilimali, Nicholas Lekule amesema mafanikio ya jukwaa hilo hayapimwi kwa maazimio yatakayofikiwa pekee, bali kwa ubora wa maamuzi, mapendekezo na hatua za pamoja zitakazochukuliwa na wadau baada ya majadiliano ili kuleta tija kwa jamii zenye raslimali asili.

Amesema jukwaa hilo ni nafasi muhimu kwa wadau kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya uziduaji, ikiwemo uwazi, uwajibikaji na utekelezaji wa sheria na mikataba inayolinda haki za binadamu na kuheshimu utawala bora katika sekta hiyo.

Amewahimiza washiriki kujadili kwa kina, kuuliza maswali magumu yanayotoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sekta hiyo ya uziduaji nchini.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya HakiRasilimali, Rose Ugulumu amewataka washiriki kutoa maoni na mapendekezo yatakayochangia maendeleo ya sekta ya uziduaji na ustawi wa Tanzania kwa ujumla.

Nao baadhi ya washiriki wa jukwaa hilo wamesema bado kuna changamoto ya uwazi na ushirikishaji wananchi katika sekta ya uziduaji, hali inayochangia malalamiko, migogoro na ukiukaji wa haki za binadamu katika maeneo yenye miradi ya uwekezaji, hivyo ni vyema wadau kusaidia wananchi katika eneo hilo.

Jukwaa hilo la siku mbili kuanzia Alhamisi, Novemba 12, 2026, linaongozwa na mjadala mkuu uliobebwa na kaulimbiu isemayo, “Kutoka Utajiri wa Rasilimali Asilia hadi Ustawi wa Pamoja: Je Tanzania Iko Tayari kwa Enzi Mpya ya Sekta ya Uziduaji?”.
Na George Binagi, BMG
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Dunford Mpelumbe.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la HakiRasilimali, Nicholas Lekule.
Washiriki kutoka taasisi mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi.

No comments:

Powered by Blogger.