LIVE STREAM ADS

Header Ads

TANZANIA YATAFUTA UFADHILI WA KILIMO HIMILIVU KATIKA COP31

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

 Pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaondelea kufanyika Jijini, Antalya, Uturuki, kwa kipindi cha 9 - 20 Novemba 2026, tarehe 11 Novemba 2026, umefanyika Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Kilimo uliolenga katika kuhamasisha ufadhili na uwekezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa ajili ya kuimarisha uhimilivu wa sekta ya kilimo.

Mkutano huo uliwakutanisha wawakilishi kutoka Serikalini, taasisi za fedha, sekta binafsi na washirika wa maendeleo duniani kujadili mikakati ya kuongeza upatikanaji wa fedha za miradi ya kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi  katika mifumo ya chakula na kuhakikisha  wakulima hasa wanawake na vijana wananufaika na fursa za ufadhili huo.

 Akizungumza katika mkutano huo, mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo Bi. Zaninabu T. Sheuya, Mkurugenzi wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo katika kuongeza uwekezaji wa kilimo himilivu na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha fedha za Mabadiliko ya Tabianchi zinapatikana kwa wingi na kutoa kipaumbele kwa wakulima wanaoathirika moja kwa moja.

Aidha, Bi. Prudence Masako, Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya CARE Tanzania alitoa wito kwa Wadau  kuendelea  kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuongeza uwekezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi yenye matokeo chanya ili kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wakulima wadogo ili kuimarisha uchumi endelevu.

Ufadhili wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi utawezesha kuchochea utekelezaji wa vipaumbele vya Dira 2050 katika sekta ya kilimo kwa kuelekeza rasilimali katika uwekezaji  unaochangia maendeleo ya kilimo chenye tija, shindani na himilivu kwa athari za mabadiliko ya tabianchi. 

No comments:

Powered by Blogger.