WAZIRI SANGU AMPA POLE ASKOFU BEATUS URASSA KUFUATIA KIFO CHA PADRI GODRICK MUNDEWA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Na OWM (KAM), Sumbawanga
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amemtembelea Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, Mhashamu Askofu Beatus Urassa (ALCP/OSS), na kumpa pole kufuatia kifo cha Padre Godrick Mundewa aliyefariki baada ya ajali iliyotokea Oktoba 30, 2026.
Akitoa salamu za pole, Sangu amesema kifo cha Padre Mundewa kimeacha pengo kubwa kwa Kanisa na jamii kwa ujumla kutokana na mchango wake katika huduma za kiroho na ustawi wa jamii.
Waziri Sangu amemweleza Askofu Urassa kuwa ziara yake mkoani Rukwa ni kwa niaba ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, katika Mahafali ya 17 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mtakatifu Theresia, Sumbawanga.
Katika mahafali hayo, Waziri Sangu ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni litakalochukua wanafunzi 156, sambamba na kuendesha harambee ya kuchangia ujenzi huo.
Katika hatua nyingine, Sangu amemshukuru Askofu Beatus kwa kutoa kibali cha Misa Takatifu ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, iliyofanyika Sumbawanga Oktoba 14, 2026, sambamba na kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Naye, Askofu Urassa ameshukuru kwa ujio huo, akisema uwepo wa Waziri katika shughuli za Kanisa ni muendelezo wa ushirikiano na mahusiano mazuri kati ya Kanisa Katoliki na Serikali.
"Ninaomba umfikishie salamu Rais Samia Suluhu Hassan kwa michango yake ya hali na mali kuwezesha shughuli mbalimbali za Kanisa tangu alipoingia madarakani," amesema Askofu Urassa.
Waziri Sangu amefanya ziara hiyo mkoani Rukwa katika kutekeleza jukumu lake la mahusiano kati ya Serikali na makundi ya kijamii, ikiwemo madhehebu ya dini.











No comments: