ITWANGI YANG'ARA! MASUNULA YAONGOZA SHINYANGA, YAIBUKA YA PILI KITAIFA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Tazama Matokeo ya MASUNULA
Na Kadama Malunde – Shinyanga
Shule ya Msingi Masunula iliyopo katika Jimbo la Itwangi, Wilaya ya Shinyanga, imeendelea kuandika historia katika sekta ya elimu nchini baada ya kufanya vizuri katika Matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2026, na kushika nafasi ya pili kati ya shule 10 bora za msingi Tanzania.

Mafanikio hayo yanaifanya Masunula kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri zaidi nchini, huku ikiendelea kuthibitisha ubora wa elimu inayotolewa katika shule za Serikali.
Kwa mujibu wa orodha ya shule 10 bora za msingi nchini mwaka 2026, Masunula imeshika nafasi ya pili kwa kupata wastani wa alama 285.5172, nyuma ya Shule ya Msingi Kemebos ya Bukoba iliyoshika nafasi ya kwanza kwa wastani wa alama 285.7333.
Katika matokeo hayo, jumla ya wanafunzi 29 wa Masunula waliofanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 17 na wavulana 12, wote wamepata Daraja A (Bora), sawa na asilimia 100 ya ufaulu.
Mafanikio hayo yanaifanya Masunula kuwa kinara wa shule za msingi katika Wilaya ya Shinyanga, ikiongoza shule nyingine za Serikali na binafsi zilizopo wilayani humo katika matokeo ya mwaka huu.
Uchambuzi wa matokeo unaonesha kuwa wanafunzi wa Masunula wamefanya vizuri katika masomo yote sita, huku Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi likiongoza kwa wastani wa alama 49.5517 kati ya 50.
Likifuatiwa na Hisabati (49.5172), Uraia na Maadili (47.9310), Sayansi na Teknolojia (47.5862), English Language (46.8966) pamoja na Kiswahili (44.0345).
Jambo la kipekee ni kwamba masomo yote sita yameingia katika kundi la Daraja A (Bora), jambo linalodhihirisha juhudi za walimu na wanafunzi katika kuhakikisha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji katika kila somo.
Aidha, kupata ufaulu wa asilimia 100 kwa wanafunzi wote 29 waliofanya mtihani huo ni mafanikio makubwa yanayoweza kuwa mfano wa kuigwa kwa shule nyingine nchini.
MASUNULA YAONGOZA SHINYANGA, SHULE TISA ZINGINE ZAINGIA 10 BORA
Katika orodha ya shule 10 bora za Wilaya ya Shinyanga kwa matokeo ya PSLE 2026, Masunula imeongoza kwa wastani wa alama 285.5172.
Shule nyingine tisa zilizofanikiwa kuingia katika orodha hiyo ni St. Maria Goretti iliyoshika nafasi ya pili kwa wastani wa alama 269.3846, Shilabela nafasi ya tatu (268.1852), Kimandaguli nafasi ya nne (266.3864), Salawe nafasi ya tano (262.3939), Ikonda nafasi ya sita (259.8571), Kilimawe nafasi ya saba (257.1875), Kihongwe nafasi ya nane (254.0714), OLA nafasi ya tisa (252.6667) na Sumbigu iliyoshika nafasi ya kumi kwa wastani wa alama 252.0000.
Matokeo hayo yanaonesha namna shule mbalimbali katika Wilaya ya Shinyanga zinavyoendelea kufanya vizuri, huku Masunula ikiongeza heshima ya wilaya hiyo katika ramani ya elimu nchini.
AZZA ATOA PONGEZI, AAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SHULE
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, amewapongeza walimu, wanafunzi, wazazi na viongozi wa shule hiyo kwa mafanikio makubwa waliyoyapata, akisema ni matokeo ya kujituma, nidhamu na ushirikiano wa wadau wa elimu.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad
Mhe. Azza amesema mafanikio ya Masunula ni jambo la kujivunia kwa Jimbo la Itwangi na Wilaya ya Shinyanga kwa ujumla, akibainisha kuwa shule hiyo imekuwa ikionesha kiwango kizuri cha ufaulu katika mitihani ya kitaifa kwa miaka mbalimbali.
“Ninaipongeza shule hii, kwa miaka mingi imeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya taifa. Haya ni matokeo ya juhudi kubwa za walimu, wanafunzi na wazazi. Kama Mbunge wenu, nitaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha miundombinu ya shule zetu inaboreshwa zaidi ili kila mwanafunzi wa Itwangi apate mazingira bora ya kujifunzia,” amesema Mhe. Azza.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kuwa chachu kwa shule nyingine katika jimbo hilo kuongeza juhudi, kuimarisha usimamizi wa elimu na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha ufaulu.
SHULE ZA SERIKALI ZATHIBITISHA UWEZO WA KUTOA ELIMU BORA
Mafanikio ya Masunula yanatoa ujumbe muhimu kuwa shule za Serikali zina uwezo mkubwa wa kutoa elimu bora na kushindana katika viwango vya juu kitaifa.
Ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi, wazazi, Serikali na wadau wengine wa elimu ni miongoni mwa nguzo muhimu zinazoweza kuleta matokeo makubwa katika sekta hiyo.
Kwa kushika nafasi ya pili kitaifa na kuongoza shule za Wilaya ya Shinyanga, Masunula imeendelea kuinua hadhi ya elimu ya Jimbo la Itwangi na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.
Hongereni walimu, wanafunzi, wazazi, uongozi wa shule na wadau wote wa elimu wa Masunula kwa mafanikio haya makubwa.




No comments: